Ahadi, changamoto na uhalisia wa utawala wa Kenya kwanza
Rais Ruto anapotimiza siku 1000 madarakani, Taifa linajikuta katika njia panda wengi wakibaki kujiuliza maswali kuhusu utawala wake Ruto na ikiwa mwelekeo wa taifa unalingana na ahadi alizozitoa kabla ya uchaguzi.

Rais Ruto anapotimiza siku 1000 madarakani, Taifa linajikuta katika njia panda wengi wakibaki kujiuliza maswali kuhusu utawala wake Ruto na ikiwa mwelekeo wa taifa unalingana na ahadi alizozitoa kabla ya uchaguzi.
Alipochukua hatamu mwaka wa 2022, Ruto alibeba matumaini ya mamilioni ya watu waliovutiwa na mfumo wake wa kiuchumi wa "bottom-up" waliotarajia ungebadilisha maisha yao.
Manifesto yake ya kampeni ilikuwa ya kuvutia ;alijitaja kuwa kiongozi mchapakazi na anayeelewa hali halisi ya maisha ya raia hasa wale wa tabaka la chini na kujipa jina la umaarufu “hustler “akiahidi kuunda nafasi za ajira kwa vijana na kuwapa kupaumbele watu wa kipato cha chini.
Miaka miwili na nusu baadaye, Ruto ambaye alikuwa ameahidi kupigana na ufisadi anajipata akiwa amepachikwa majina ya kejeli na wakosoaji wake kama Zakayo,kasongo na mengineyo kwa kumtania kwa kiu yake ya kuanzisha ushuru zaidi na ahadi zisizotekelezwa.
Katika bajeti yake ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2023/2024, serikali ya Kenya Kwanza ilitekeleza mageuzi mapya ya ushuru, ikiwemo kuongezwa kwa kiwango cha ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.
Mapato ya wafanyakazi yalipungua kwa kiasi kikubwa baada ya kuanzishwa kwa makato mapya, ikiwemo asilimia 15 ya ushuru wa nyumba, asilimia 2.7 kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) na ongezeko la makato kwa Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).
Hatua nyingine za ushuru katika Mswada wa Fedha wa 2024 zilisababisha maandamano makubwa kote nchini.
Maandamano haya, ambayo yaliongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Kenya, wanaofahamika kwa jina maarufu “Gen z “yalimlazimu Rais Ruto kuondoa mswada huo, jambo ambalo lilikuwa pigo kubwa kisiasa na linaonyesha kiwango cha juu cha kuchoshwa kwa umma.
Mwamko huu wa vijana pia ulionyesha kuwa kizazi kilekile alichodai kukitetea ndicho kilichogeuka kuwa wakosoaji wake wakuu.
Kenya Kwanza iliahidi kujenga nyumba 250,000 kila mwaka.Baada ya kuingia mamlakani, idadi ya nyumba ilipunguzwa kuwa 2000 kila mwaka.
Baada ya siku 1000 nyumba 11,000 pekee zimekamilika huku 148,165 zikiew zinajengwa.Huu ni upungufu mkubwa ikilinganishwa na lengo la nyumba 500,000 kuwa zimekamilika kufikia Aprili 2025.
Mpito kutoka hazina ya kitaifa wa Bima ya Afya( NHIF) hadi Mfumo wa Bima ya Afya ya Jamii (SHA) umekumbwa na matatizo mengi katika utekelezaji.Licha ya kulipa michango ya kila mwezi, wagonjwa hawawezi kupata matibabu kwa wakati kutokana na kufeli kwa mifumo.
Ripoti ya Chama cha Hospitali za Kibinafsi (RUPHA) ilionyesha kuwa taasisi tisa kati ya kumi za umma na binafsi zinakabiliwa na changamoto za kukidhi gharama zao kutokana na kuchelewa kwa malipo kutoka SHA huku wahudumu wa afya wakiendelea kufanya migomo kila mara wakilalamikia ajira.
Serikali Kenya Kwanza iliahidi kuajiri walimu 116,000 ndani ya miaka miwili ya kifedha.
Waliahidi pia kuboresha uwezo wa shule za sekondari za kutwa ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na kupunguza gharama ya elimu.
Hata hivyo, serikali imekuwa ikikumbwa na changamoto za kifedha katika kugharamia elimu katika shule za umma. Waziri wa Elimu Julius Migos alkisema kuwa serikali inadaiwa na shule Sh64 bilioni.
Kampeni ya Rais Ruto pia ilijikita sana katika kuhimiza biashara ndogo ndogo kupitia upatikanaji wa fedha za mikopo.
Hustler Find amayo ilianzishwa mwezi Novemba 2022, ililenga kutoa mikopo ya nafuu kwa biashara ndogo ndogo.
Hata hivyo, mpango huo umekumbwa na changamoto kadha.
Katika mwaka wake wa kwanza, ulipokea KSh12 bilioni, lakini mgao wa fedha ulianza kupungua hadi KSh800 milioni mwaka 2024 na KSh1 bilioni katika mwaka wa fedha ujao, ikiwa ni mbali sana na kiasi kilichokuwa kikiombwa cha KSh5 bilioni.
Aidha, mpango huu umekumbwa na changamoto za kutolipwa kwa mikopo, na hivyo serikali inaangalia uwezekano wa kufuta KSh6 bilioni ya mikopo isiyolipwa iliyochukuliwa na Wakenya milioni 10.
Rais Ruto alijitolea kupambana na ufisadi. ‘Nikipata fursa ya kuendesha serikali, hakutakuwa na ufisadi kwa sababu hakutakuwa na pesa ya kuiba kwani kila senti itatumika.
Hakutakuwa na senti inayozunguka mahali popote kwa mtu kuiba.”
Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani, kashfa kadhaa zimetikisa serikali ya Kenya Kwanza.
Ikiwa ni pamoja na zabuni ya vyandarua ya Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa na Vifaa vya Matibabu Kenya (Kemsa) ambapo mamilioni ya pesa ziliporwa na maafisa wa serikali wasio waaminifu.
Kenya kwanza pia imekumbwa na visa vya mauaji ya kiholela ya raia na utekaji nyara na unyanyasaji wa raia.
Hata baada ya rais kuahidi kuwa visa hivyo havitakuwepo, mauaji yanazidi kushuhudiwa kisa cha hivi punde kikiwa cha Albert Ojwang ambaye anashukiwa kuuwawa na polisi katika kituo cha polisi.
What's Your Reaction?






