Ubalozi wa Marekani wataka uchunguzi wa kina wa kifo cha Ojwang'

Kupitia taarifa fupi iliyotolewa siku ya Jumatano, ubalozi wa Amerika ulisema unaunga mkono wito wa uwajibikaji na uwazi katika uchunguzi unaoendelea.

Jun 12, 2025 - 11:43
Jun 12, 2025 - 16:00
 0  6
Ubalozi wa Marekani wataka uchunguzi wa kina wa kifo cha Ojwang'

Ubalozi wa Amerika jijini Nairobi umeitaka serikali ya Kenya pamoja na Mamlaka Huru ya kusimamia utendakazi wa polisi (IPOA) kuhakikisha uchunguzi wa haraka, wa wazi, na wa kina kuhusu kifo cha mwanaharakati Albert Ojwang, ambaye alifariki katika hali tata akiwa mikononi mwa polisi.

 Ubalozi huo ulituma rambirambi zake kwa familia ya Ojwang.

“Ubalozi wa Amerika nchini Kenya unatuma rambi rambi kwa familia na wapendwa wa Albert Ojwang’ katika kipindi hiki cha majonzi.”

Kupitia taarifa fupi iliyotolewa siku ya Jumatano, ubalozi wa Amerika ulisema unaunga mkono wito wa uwajibikaji na uwazi katika uchunguzi unaoendelea.

“Kwa kuzingatia wasiwasi kuhusu mazingira ya kifo cha Ojwang’, Ubalozi unaunga mkono wito kutoka kwa serikali, wabunge, na wananchi wa Kenya wa kutaka uwajibikaji kupitia uchunguzi ulio wazi.”

“Ubalozi unahimiza Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuendesha uchunguzi wake kwa haraka na kwa kina. Tunaitaka pia serikali ya Kenya kuhakikisha IPOA inapata usaidizi na taarifa inazohitaji kutekeleza majukumu yake.”

Ojwang alifariki tarehe 8 Juni 2025, siku moja baada ya kukamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliodai kuwa wanamchunguza kuhusiana na chapisho alilodaiwa kuweka kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Baadaye alisafirishwa hadi Nairobi na kuzuliliwa katika kituo cha polisi cha Central.

Siku moja baadaye polisi walidai kuwa Ojwang alipatikana akiwa amefariki kutokana na maumivu ya kichwa aliyojisababishia.

Lakini uchunguzi wa maiti uliofanywa na wanapatholojia waliotoa ripoti ya pamoja ulibaini kuwa Ojwang alikuwa na majeraha mabaya ya kichwa ,shinikizo shingoni pamoja na majeraha mengine.

“Tulipata majeraha kwenye kichwa, dalili ya majeraha shingoni na sehemu zingine mwilini na miguuni.”

What's Your Reaction?

Like Like 0
Dislike Dislike 0
Love Love 0
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0